Wednesday, May 20, 2020

Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa Amuomba Radhi Abdulrahman Kinana Kwa Kumkashifu na Kumchafua Kwa Tuhuma za Ujangili



Mbunge wa Iringa Mjini, 
Peter Msigwa amemwomba radhi Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kutokana na kauli za uongo alizowahi kuzitoa dhidi yake.

Katika nyakati tofauti, ndani na nje ya Bunge, Mchungaji Peter Msigwa aliwahi kutoa kauli za uzushi dhidi ya Kinana, akimtuhumu kujihusisha na ujangili na biashara ya nyara za serikali.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema tuhuma zote alizowahi kuzitoa dhidi ya Kinana bungeni na kwenye mikutano ya kisiasa nje ya Bunge, hazikuwa na ukweli wala ushahidi wowote.

"Natoa tamko la kumuomba radhi Abdulrahman Kinana, ikumbukwe nilikuwa na kesi katika mahakama Kuu ya Tanzania iliyofunguliwa na Kinana kutokana na matamshi niliyowahi kuyatoa kumuhusisha na ujangili. Ninakiri tuhuma hizo hazikuwa za kweli, zilikuwa na malengo potofu

“Ni dhahiri kwamba nimemkosea, nimemdhalilisha na kumkashifu ndugu yangu Abdulrahman Kinana. Nimekutana na kuzungumza naye kuhusu jambo hili na kumwomba radhi. Ninashukuru kwamba amekubali kunisamehe.

“Bila shaka mtakubaliana nami kwamba Kinana ni mzalendo, muungwana na mstaarabu ambaye kwa kweli hastahili kukashifiwa wala kudhalilishwa.

"Nitaendelea kumheshimu kama alivyodhihirisha ustahimilivu na uungwana wake kwangu, kwa familia yangu na kwa Watanzania," Mchungaji Msigwa alisema.

Mahakama Kuu ya Tanzania, kupitia kesi namba 108 ya mwaka 2013, ilimkuta Mchungaji Msigwa na hatia ya kuandaa na kutoa kashfa dhidi ya Kinana kwa malengo ya kisiasa, kumchafulia jina na kumshushia hadhi yake katika jamii; ndani na nje ya nchi.

Kabla ya kupeleka suala hilo mahakamani, Kinana kupitia kwa Wakili wake, Erick Sikujua Ng’maryo, alimtaka Mchungaji Msigwa kufuta kauli zake hizo na kuomba radhi hadharani kwa kuwa hazikuwa na ukweli wowote. Mbunge huyo alikataa kufanya hivyo na kusema yuko tayari kujitetea mahakamani.

Monday, May 18, 2020

Wagonjwa Wa Corona Kenya Wafika 887 Baada ya Wengine 57 Kuongezeka



Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi kufikia 887 baada ya wagonjwa wengine 57 kukutwa na virusi hivyo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wagonjwa hao ni wanawake 23 na wanaume 34 wote wakiwa kati ya umri wa miaka miwili na 61.

Katika taarifa iliotolewa na wizara ya Afya siku ya Jumapili, Msemaji wa serikali Cyrus Oguna alisema kwamba kati ya wagonjwa hao wapya mjini Mombasa , Nairobi 17 , kajiado 3 huku Kwale na Kitui zikitangaza wagonjwa mmoja mmoja mtawalia.


 Idadi ya vifo ni 50 na waliopona wamefikia 313.

Sunday, May 17, 2020

BREAKING: Rais Magufuli Kasema Wagonjwa Wa Corona Nchini Tanzania Wamepungua Sana...Kasema Hali Ikiwa Hivi Wiki Ijayo Huenda Vyuo Vikafunguliwa


Rais John Magufuli amesema kuwa idadi ya wagonjwa wa Corona nchini Tanzania imepungua sana, huku baadhi ya vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wenye maambukizi vikiwa vitupu.

Rais amesema hilo wakati akitoa salamu kwa Watanzania alipohudhuria ibada ya Jumapili- KKKT Usharika wa Chato Mkoani Geita,

Akitoa takwimu hizo Rais Magufuli amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam;

Amana ilikuwa inalaza wagonjwa 198 leo walikuwepo watu 12 walioathirika, Mloganzila walikuwa watu 30 leo 6, Kibaha huwa wanalazwa watu zaidi ya 50 leo wamebaki watu 22 ambao hali zao ni nzuri.

Akitaja vituo vingine amesema Aga Khan wamebaki watu 31, Hindu Mandali wamebaki 16, Regency 17, TMJ wamebaki 7, Rabininsia wamebaki 14.

Katika mikoa mingine amesema, Arusha kuna vituo vitatu, Moshono kuna wagonjwa 11, Longido na Karatu hakuna mgonjwa.

Mwanza kuna vituo 10 ambapo Buswelu kuna wagonjwa 2, Misungwi 2 Ukerewe, Magu, Mkuyuni, Bachosa, Sengerema, Kwemba kote hakuna mgonjwa, huku Hospitali ya Bungando na Sékou Touré kuna wagonjwa 2 wenye uhitaji maalum.

Dodoma kuna vituo vinne ambapo mjini viko viwili kuna wagonjwa wawili huku Kongwa na Kondoa kukiwa hakuna hakuna mgonjwa

Tuesday, May 12, 2020

Spika Ndugai Atoa Masharti Ya Kumtimua Bungeni Cecil Mwambe




Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, 
amewataka wale wote wanaotaka amfukuze Ubunge Mbunge wa Ndanda Cecil Mwambe, basi wamshauri amuandikie Spika barua ya kujiuzulu kwake, halafu waone kama ataendelea kukaa bungeni.

Spika Ndugai ameyabainisha hayo leo Mei 12, 2020 na kusema kuwa maamuzi hayo yote ya kumrejesha Mwambe bungeni, yamekuja kutokana na yeye kupata barua ya upande mmoja.

"Nimeeleza Mwambe amewahi kuniandikia barua lini?, hivi wewe ungekuwa Spika ungefanyaje, huna barua ya mtu kujiuzlu ungefanyaje?, unamfukuza tu!, lazima mchunguze na muangalie mzani uko wapi, Mwambe yupo hajafa, mwambieni aandike barua anikabidhi mimi, akishanikabidhi muone kesho yake itakuwaje" amesema Spika Ndugai.

Aidha Spika Ndugai amesema kuwa leo jioni atatolea ufafanuzi kuhusu tamko lililotolewa na CHADEMA, kwamba Wabunge wake waliojiweka karantini kwa sasa hawatorudisha posho kwa sababu wao siyo wezi

Friday, May 31, 2019

ATCL yamvuruga Nape, ahoji kucheleweshwa kwa ndege

ATCL yamvuruga Nape, ahoji kucheleweshwa kwa ndege

Serikali yakanusha kuwalazimisha wafanyakazi wake kuwa na laini ya TTCL


Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema hakuna agizo la Serikali linalolazimisha mfanyakazi wa Serikali kuwa na laini ya TTCL isipokuwa viongozi wanaowekewa vocha za Serikali kwamba ni muhimu kuwa na laini hizo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo amesema taarifa inayosambaa kwenye mitandao kuhusu hilo ni ya upotoshaji na kuwataka wananchi kuipuuza.

Wednesday, May 29, 2019

Rais Magufuli ataka Jumuiya za Kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Emmerson Mnangagwa kwa hatua madhubuti za kufanya mageuzi ya kiuchumi katika nchi hiyo na ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe.

Rais Magufuli amesema hayo wakati akitoa hotuba katika Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Rais Mnangagwa kwa heshima yake na kufanyika Ikulu Jijini Harare.

Rais Magufuli amesema katika kipindi kifupi cha tangu Rais Mnangagwa aingie madarakani hali ya uchumi imeanza kuimarika ambapo kwa sasa uchumi wa Zimbabwe unakua kwa wastani wa asilimia 3.5, mwaka ujao unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.2 na mwaka unaofuata kuongeza hadi wastani wa asilimi 4.4.

Kufuatia hali hiyo ameisihi Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe kwa kuwa vikwazo hivyo vinawaumiza wananchi wa Zimbabwe wakiwemo watoto na wanawake.

Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli kwa mara nyingine amewapa pole Rais na wananchi wote wa Zimbabwe kwa kupoteza watu takribani 400 waliofariki dunia katika mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai kilichoikumba Zimbabwe Machi 2019. Amesema Watanzania wanaungana na ndugu zao Wazimbabwe katika majonzi ya kuondokewa na jamaa zao na wanawaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina.

Kuhusu uhusiano wa Tanzania na Zimbabwe ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Robert Mugabe, Rais Magufuli amesema Tanzania inatambua na inathamini uhusiano huu wa kihistoria na kidugu na amebainisha kuwa jukumu lililopo sasa ni kuelekeza nguvu nyingi zaidi katika uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi utakaoziwezesha Tanzania na Zimbabwe kuongeza biashara na uwekezaji.

Rais Magufuli amebainisha kuwa katika mazungumzo yake ya faragha na Rais Mnangagwa leo mchana wamekubaliana kusimamia ipasavyo makubaliano yaliyopo katika Kamati ya Pamoja ya Kudumu (Joint Permanent Commission – JPC) kwa manufaa ya nchi zote mbili.

“Rais Mnangagwa ujio wangu hapa Zimbabwe ni kuthibitisha kuwa urafiki wetu bado upo imara na sisi Tanzania tumejipanga kuuimarisha zaidi, tunataka tufanye biashara zaidi na nyinyi ndugu zetu wa Zimbabwe ili tukuze uchumi wa nchi zetu na kuongeza kipato cha wananchi wetu” amesisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Rais Mnangagwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali mwaliko wake, na amemthibitishia kuwa yeye na wananchi wa Zimbabwe wanatambua kuwa Watanzania ni ndugu zao waliojitolea kwa dhati katika ukombozi wao wakiongozwa na dhamira ya dhati ya Hayati Mwl. Nyerere.

Amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwa kiongozi wa kwanza katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoa msaada wa chakula, dawa na vifaa vya kujihifadhi wakati Zimbabwe alipokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na Kimbunga Idai mwezi Machi 2019.

Rais Mnangagwa amesema msaada huo uliwagusa Wazimbabwe wengi na kuwakumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesisitiza kuwa daima Zimbabwe itabaki kuwa rafiki na ndugu wa kweli wa Tanzania na hivyo amemhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kukuza zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kushirikiana katika usafiri wa anga.

Amemshukuru Rais Magufuli kwa kumpa mbinu mbalimbali za kiuongozi ikiwemo kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali na ameahidi kudumisha ushirikiano kati ya chama chake ZANU-PF na Chama Cha Mapinduzi (CCM).