Wednesday, May 29, 2019

Makonda atangaza vita na Wamachinga wasio na vitambulisho Dar


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuanzia June 3 mwaka 2019 ni marufuku kwa Wamachinga wote wasio na vitambulisho kufanya biashara katika maeneo yote jijini Dar.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 29, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mwitikio wa wafanyabiashara kuchukua vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Rais John Magufuli kwa wakuu wote wa Mikoa nchini.

Makonda amesema Jiji hilo lilipatiwa vitambulisho 175,000 lakini wapo ambao hawajachukua hadi sasa.

Amesema kuwa atafanya msako mkali kuwatafuta wamachinga wote wasio na vitambulisho hivyo

Mbwana Samatta Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Msemaji Mkuu Wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi


SERIKALI imesema itaendelea kumsaidia kwa hali na mali Nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, anayechezea Klabu ya Genk ya Nchini Ubelgiji Mbwana Samatta ili kuhakikisha kuwa anafungua milango ya uwekezaji na kuiweka juu ramani ya Soka la Tanzania katika anga la kimataifa.
 
Akizungumza jana Jumanne (Mei 28, 2019) Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam na Nahodha huyo waTaifa Stars, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema Samatta ameonyesha njia iliyoshindwa kufikiwa na wachezaji wengi wa miaka ya nyuma waliojaribu kucheza Soka la kulipwa katika vilabu mbalimbali vya Nchi za Nje hususani Bara la Ulaya.
 
Dkt. Abbasi alisema Serikali ilimteua Sammatta kuwa Balozi wake wa Utalii kutokana na sifa kubwa zilizoletwa na mchezaji huyo nje ya mipaka ya Tanzania kwa kuwa Serikali ina Imani naye kubwa katika kufungua milango ya fursa za uwekezaji hususani katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano hapa nchini. 
 
“Mbwana Samatta ameonyesha njia ambayo ilikuwa ndoto iliyoshindwa kutimizwa na wachezaji wengi wa zamani, hatua hii aliyofikia ni kubwa na imetokana na sifa kubwa ya nidhamu na kipaji cha mchezo huu hili ni funzo kwa wachezaji wetu chipukizi” alisema Dkt. Abbasi.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema kwa sasa yapo mambo makubwa na mazuri hususani vivutio vya sekta ya utalii, hivyo kupitia nafasi yake ya Ubalozi Serikali itatoa msaada wowote unaohitajiwa na mchezaji huyo ili kuhakikisha kuwa vivutio vya Tanzania vinabainishwa na hivyo kutangaza mambo mazuri ya Tanzania.
 
Aidha Dkt. Abbasi alisema Ofisi yake imeandaa mikakati mbalimbali ya mawasiliano ya kitaifa katika kuisema nchi katika maeneo mbalimbali hivyo kumtaka mchezaji huyo kutumia majukwaa hayo kwa ajili ya kuona namna bora ya kutumia fursa hizo ili kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alimtaka mchezaji huyo kuwasiliana naye iwapo kutakuwepo na changamoto yoyote anayoweza kuipata katika kutekeleza majukumu yake ya nafasi ya Ubalozi kwani kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imefungua milango ya ushirikiano na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
 
Kwa upande wake, Nahodha huyo wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alisema akiwa nchini Ubelgiji tayari amefanya juhudi kubwa katika kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, ambapo mwanzoni mwa mwezi ujao madaktari 5 wa timu hiyo wanatarajia kuja nchini kwa ajili ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii nchini.
 
Samatta alisema raia wengi wa kigeni wana shauku ya kutembelea Tanzania kutokana kusikia na kuona uzuri wa vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Wanyama, hivyo akiwa Balozi wa Utalii afanya kila liwezekanalo  kukaa karibu na viongozi na wachezaji wa klabu yake ya KRC Genk kuwaeleza uzuri wa Tanzania ili na wao waonesha nia ya kuitembelea Tanzania.
 
“Wachezaji wengi hususani wale wa kiafrika waliopo nje hususani Bara la Ulaya wanaipenda sana Tanzania, na hi inatokana na sifa tuliyonayo, na hivyo kwa kutumia nafasi yangu ya Ubalozi nitaendelea kushawishi waitembelee Tanzania” alisema Samatta.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Samatta Tours, Hamis Waziri aliishukuru Serikali kutokana na jitihada mbalimbali inazofanya kwa ajili ya kuhamasisha sekta ya utalii nchini na kusema taasisi hiyo itakuwa tayari kutangaza matukio mbalimbali kwa ajili ya kulitangaza jina la Tanzania.

NACTE Yasitisha Udahili Kozi Ya Hudumu Ya Afya Ngazi Ya Jamii Kwa Mwaka Wa Masomo 2019/2020


Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi(NACTE)limetangaza kusitisha udahili wa wanafunzi wapya wa program ya Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii(Community Health) kwa mwaka wa masomo 2019/2020 hadi hapo itakapotangaza tena.

Akizungumza mbele ya wanahabari Jijini Dodoma  janas Mkurugenzi wa uzingativu, ufuatiliaji na Tathmini wa NACTE Jofrey Oleke, amesema maombi ya udahili kwa waombaji wapya wa Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2019/2020, umesitishwa hadi hapo baraza litakapotangaza maamuzi mengine.

Kufutwa kwa udahili huo kumetokana na maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwamba kwa mwaka huu wa masomo hakutakuwa na kozi hizo.

Kuhusu kusitishwa kwa udahili, amesema baraza limepokea maagizo kutoka wizara ya afya ambao ndio wanaosimamia kozi zote za afya, kuwa katika mwaka huu wa masoma hakutakuwa na udahili katika ngazi hiyo afya ya jamii nasi tunatekeleza.

“Baraza linavitaarifu vyuo na umma kwamba udahili wa wanafunzi katika programu ya Huduma ya afya Ngazi ya Jamii umesitishwa hadi hapo itakapotangazwa tena”,amesema.

Pia baraza limetangaza kufunguliwa kwa udahili mpya kwa ngazi za Astashahada na stashahada kwa kozi zote isipokuwa kwa kozi za ualimu na utaendelea mpaka tarehe 2 mwezi wa tisa mwaka huu kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo katika ngazi hizo.

Amefafanua kuwa kwa waombaji wa programu za Afya katika vyuo vya Serikali watatakiwa ama kuomba moja kwa moja kupitia vyuoni ambapo vyuo vitasawasajili kupitia baraza la chuo au wanaweza kuomba kupitia tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (www.nacte.go.tz) kubonyeza kwenye ‘apply online'(SAVS).

Kuhusu waombaji wa programu za Afya kwenye vyuo visivyo vya Serikali na waombaji wa programu nyingine zote wanatakiwa kuomba moja kwa moja kwenye vyuo husika.

“Hivyo vyuo vitapokea maombi na kufanya uchaguzi wa wanafunzi wenye sifa na kisha wawasilishe NACTE majina ya waliochaguliwa kwa ajili ya uhakiki kabla ya kuyatangaza, vyuo vinaelekezwa kuzingatia utaratibu wa udahili kama ulivyotolewa na baraza katika mwaka wa masomo 2019/2020,”amesema.

Amewataka wahitimu wote wa Elimu ya Sekondari na vyuo wenye sifa za kujiunga na kozi za Astashahada na Stashahada, kufanya maombi kwa umakini ili kuweza kupata nafasi ya kujiunga programu wanazozipenda na ambazo wanatimiza vigezo/sifa za kujiunga nazo kwa mwaka 2019/2020.

Pia baraza limewashauri waombaji na wazazi kuhakikisha kuwa wanaomba kwenye vyuo vinavyokidhi ubora ambavyo vimeorodheshwa kwenye kitabu cha mwongozo wa udahili kwa mwaka wa masomo mwaka 2019/2020 .